Nishati Jadidifu

Makala ya nishati jadidifu1

Jukwaa linalojihusisha na Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi (Forum CC)-Tanzania na Pan African Climate Justice Alliance (PACJA) wanatekeleza mradi wa pamoja kuboresha ushiriki wa Asasi za kiraia katika utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano ya Paris wa 2015 na kuhamasisha ushiriki wa wadau katika Mapendekezo ya Kitaifa ya utekelezaji wa Makubaliano ya Paris na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu hadi ifikapo 2030.

Katika majukumu ya utekelezaji wa mradi, Forum CC walitembelea kikundi cha wanawake kinachoitwa Fahari Yetu kilichopo sokoni Tabata Muslim mtaa wa Tabata Msimbazi kinachojishughulisha na utengenezaji wa mkaa wa taka ngumu zitokanazo na mabaki ya mazao (mkaa mbadala).

Kikundi cha Fahari Yetu ni moja ya vikundi vinavyofanya kazi na Forum CC katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (hasa lengo 7, 12 na 13) ili kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia utengenezaji wa nishati mbadala kwa kutumia malighafi ya taka za mazao.

 Kikundi cha Fahari Yetu kina jumla ya wanachama 11 ambao miaka yao ni kati ya miaka 70 na 24 wote wakiwa wakina mama. Tangu mwaka 2019 wanakikundi wamekuwa wakijihusisha na utengenezaji mkaa wa taka kwa kupitia fursa ya mafunzo chini ya Forum CC yaliyotolewa na mtaalamu Baraka Machumu kutoka Shirika la Green Conservers.

Kupitia uzalishaji wa mkaa wa taka, kikundi cha Fahari Yetu kimepata faida nyingi za kijamii, kiuchumi, kiafya na pia kimeweza kuchangia juhudi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwenye jamii kama kupunguza kilo 100 za taka ngumu kutoka kwenye eneo lao kila siku kwa ajili ya kutengenezea mkaa wa taka, hivyo kupunguza gharama za kulipia taka kiasi cha shilingi 1,000 kila siku.

 Matumizi ya mkaa wa taka kupikia yamewasaidia wanawake hao kuimarisha afya zao dhidi ya nishati nyingine duni zenye moshi (kuni) ukizingatia kuwa mkaa wa taka hautoi moshi. Pia kupitia mkaa huu wamepunguza gharama za matumizi ya nishati ya kupikia kutoka shilingi 5,000 hadi 2,000 kwa siku hivyo kuongeza kipato chao na kuweza kutumia kiasi hicho cha fedha katika mahitaji mengine muhimu ya kila siku.

Hadi sasa kikundi kina wateja zaidi ya 10 wanaonunua mkaa wao kila siku. Hivi sasa wateja wao wakuu ni mama lishe pale sokoni na mama wa nyumbani jirani na sokoni. Fursa hii imewapa hamasa kubwa sana wanakikundi kiasi cha kuwavutia wanawake wengine kujiunga na kikundi chao. Ndani ya mwaka 2020 wameweza kuongeza wanachama wawili kwenye kikundi chao na kuwepo kwa maombi mengi kutoka kwa wanawake hapo sokoni.

Hata hivyo, ukosefu wa vifaa bora vya uzalishaji mkaa wa taka na ukosefu wa eneo la uzalishaji na kuhifadhi malighafi na bidhaa zao ni baadhi tu ya changamoto ambazo zinarudisha nyuma juhudi za kikundi. Mwenyekiti wao ndugu Warda Omary Sera amesema “tunawaomba wadau wengi wajitokeze kutusaidia kupata vifaa vizuri vya kuzalishia mkaa wa taka ili tuweze kuongeza uzalishaji wetu. Wanawake ni nguzo kubwa katika kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa hiyo mwanamke asiachwe nyuma kwenye mijadala ya ngazi ya kijamii, kitaifa na kimataifa… kwenye hili suala hususan kwenye michakato ya utungaji wa sera na bajeti”….aliongezea.

Makala ya Nishati Jadidifu Pdf